UCHUMI WA BLUU KATIKA KUKUZA PATO LA TAIFA

27 Jun, 2022
UCHUMI WA BLUU KATIKA KUKUZA PATO LA TAIFA

Serikali imesema itaendelea kuwekeza kwenye rasilimali mafunzo kupitia Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ili kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kutumia uchumi wa bluu kuongeza pato la Taifa inatekelezwa kikamilifu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa Kitaifa kuhusu Uchumi wa Bluu jijini Dar es Salaaam, Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema  utekelezaji wa mikakati hiyo inakwenda sanjari na uzalishaji wa watalaam na utekelezaji wa miradi mikubwa ya meli ikiwemo ujenzi wa meli kubwa ya MV Mwanza na ukarabati wa meli katika Ziwa Tanganyika, Nyasa na Victoria.

‘Kama Serikali, tumejipanga kikamilifu kupitia wataalam wanaozalishwa kupitia chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), sababu Uchumi wa buluu unahitaji sana wataalam, viwanda na vifaa ambavyo ni pamoja na kuwa na meli kubwa”. amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema ni wakati muafaka kwa wataalam kuangalia nyanja zote za uchumi huo wa bluu ikiwemo viumbe vilivyopo baharini kama miti ya mikoko, mwani na vingine ili kuwa na uwanda mpana wa namna wanavyoweza kuishauri Serikali.

Kwa upande wake Balozi wa Visiwa vya Shelisheli Mhe. Maryvonne Pool amesema kama 
nchi wameweka mikakati madhubuti kuhakikisha kupitia bahari nchi inapata mapato
hali inayofanya kisiwa hicho kuwa na kiwanda kikubwa cha tatu duniani
kinachouza Samaki katika nchi za ulaya na maeneo mengine.
“Sisi tulishaanza kuitumia fursa ya uchumi wa bluu na mikakati tuliyojiwekea 
imeanza kuzaa matunda kwani Bahari imekuwa ikichangia sehemu kubwa ya pato la Nchi
yetu na kwenye hili tunalisimamia kwa karibu sababu tumeweka kanuni ambazo kwa mtu anayebainika
anafanya uvuvi haramu faini ni kuanzia dola milioni moja’ Amesema Balozi
Maryvonne
Pool

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya DMI Nahodha Ernest Mihayo ameiomba Serikali kukitazama 
chuo kwa uzito mkubwa kwani ni chuo pekee kinachozalisha wataalam watakaoweza
kutimiza lengo la Serikali katika Uchumi wa Buluu.

Mkutano huo wa kitaifa wa Uchumi wa Buluu utafanyika kwa siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine utajadili na kuangalia fursa zilizopo bahari ya Hindi na Maziwa nchini

Balozi wa Seychelles nchini Tanzania Mhe. Maryvonne Pool (Kulia) akiteta na Naibu Waziri Mhe. Mwakibete (Kushoto) wakati wa Kongamano la Uchumi wa Bluu

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete (Kulia) akibadilishana jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana (DMI) Capt. Ernest Bupamba wakati wa kongamano la Uchumi wa Bluu.

Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Mhe. Suleiman Masoud Makame – Kutoka Serikali ya Zanzibar (Kuli) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi – DMI Capt. Bupamba siku ya kufunga Kongamano la Uchumi wa Bluu.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Dr. Tumain Gurumo (Kulia), Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Mhe. Suleiman Makame (Katikati) na Mwenyekiti wa Bodi – DMI (Kushoto) wakifuatilia mada katika kongamano la Uchumi wa Bluu

Washiriki wa Kongamano la Uchumi wa Bluu ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa
wa Mwl. Julius Nyerere wakifuatilia mada mbalimbali